TAARIFA HUKUJUZA MENGI YA ULIMWENGUNI

Ijumaa, 10 Machi 2017

Mahakama yamuondoa madarakani rais wa Korea Kusini Park Geun-hye

Hakuna maoni


Mahakama ya juu nchini Korea Kusini imeunga mkono uamuzi wa bunge wa kumuondoa rais wa taifa hilo Park Geun-hye mamlakani.

Mahakama hiyo ya kikatiba imesema kuwa bi Park alikiuka sheria na kuharibu demokrasia.
Park ambaye ndio mwanamke wa kwanza kuwa rais nchini humo alihusishwa na kashfa ya kujipatia fedha kwa njia za ufisadi kutoka makampuni makubwa nchini humo na rafikiye mkubwa Choi Soon-Sil.

Bi Park huenda akakabiliwa na mashataka ya uhalifu.

Uamuzi huo ulipokelewa kwa shangwe katika maeneo mbali mbali yalio na wapinzani wa rais huyo.
Lakini wafuasi wake pia walionekana na kumekuwa na mzozano kati ya makundi hayo mawili.
Rais huyo sasa amepokonywa uwezo wa kutoshtakiwa na sasa anaweza kusimamishwa kizimbani na kufunguliwa mashtaka.

Bi Park alikuwa amesimamishwa kuhudumu kama rais tangu mwezi Disemba huku waziri mkuu wa taifa hilo akichukua majukumu ya kuongoza taifa.

Bi Choi wakati huohuo ameshtakiwa kwa kuchukua hongo kwa madai ya kuyashinikiza makampuni makubwa kumpa pesa huku akiahidi kwamba kampuni hizo zitapendelewa na serikali.

Jopo la majaji wanane katika mahakama ya kikatiba liliangazia mashtaka yanayomkabili bi Park na kuamua kwamba kulikuwa na sababu mwafaka za kumwachisha kazi.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni