SERIKALI imetangaza kuwasaka na kuwafikisha katika vyombo vya dola
wafanyabiashara wa mitaani wanaokopesha fedha kwa riba bila kuwa na
leseni ya biashara hiyo.
Pamoja na wafanyabiashara hao, Waziri wa Katiba na Sheria Dk Harrison
Mwakyembe ameomba wananchi wasaidie kuwafichua polisi na Mahakimu
wanaowapa nguvu wafanyabiashara hao kinyume na sheria.
Akizungumza na wanahabari jana mjini Iringa, Dk Mwakyembe alisema
baada ya kuwasili mjini Iringa juzi kikazi aliwafuata akinamama watano
waliolalamikia watu binafsi wenye fedha wanaofanya biashara hiyo ambao
walilalamika kutozwa riba kwa mikopo wanayochukua jambo linalowatia
umasikini.
Dk Mwakyembe alisema kwa mujibu wa sheria namba 5 ya 2006 ni kosa la
jinai kwa mtu yoyote kufanya biashara ya kukopesha fedha bila kuwa na
leseni ya biashara hiyo inayotakiwa kulipiwa kodi.
“Baada ya kufikishwa mahakamani na kupatikana na hatia, adhabu kwa
mtu anayepatikana na kosa hilo ni ama kifungo cha miaka mitano jela au
faini ya shilingi milioni 20,”alisema.
Wakati sheria hiyo ikiwa wazi, alisema amepokea taarifa kutoka kwa
akinamama hao kwamba wapo baadhi ya polisi wa mjini Iringa kwa sababu
wasizozifahamu wamekuwa wakizifanya kesi zinazohusu mikopo hiyo kuwa za
jinai badala ya madai.
“Pamoja na askari hao kuna Mahakimu, wanaoshirikiana na
wafanyabiashara hao kutengeneza mikataba ya mikopo hiyo na kusimamia
kesi zake pale, waombaji wa mikopo wanaposhindwa kulipa,” alisema.
Alisema kwa nguvu ya askari na Mahakimu hao, wanaoshindwa kulipa
mikopo hiyo hunyang’anywa mali zao na watu wenye benki hizo alizoziita
benki kanjanja na kuuzwa kwa watu wengine jambo linalozidisha umasikini
kwa wajasiriamali hasa wanawake.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema taarifa hizo hazijawahi
kufikishwa ofisini kwake na ataitumia taarifa hiyo ya waziri kutoa
maelekezo ya kuzishughulikia.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni