Jumapili, 29 Januari 2017
WAOKOAJI GEITA WAMEFANIKIWA KUWASILIANA NA WALIOFUKIWA
WAKATI imeelezwa kuwa waokoaji katika mgodi wa dhahabu wa RZ Union ulioko Geita , wamebakiza mita tatu kuwafikia waliofukiwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Medard Kalemani akizungumza na ndugu wa watu waliofukiwa amesema kwamba wanafanya mpango wa kuwapelekea chakula wachimbaji hao.
Amesema kwamba jana wamefanikiwa kufanya mawasiliano na wachimbaji hao na kwamba wapo kumi na watano na kuwa wanachohitaji kwa sasa ni chakula.
Alisema waokoaji walifanikiwa kuwafikishia kamba na kalamu watu hao ambao waliandika mahitaji yao na kusema kwamba wote wapo salama.
Awali akizungumza na gazeti hili akiwa eneo la tukio jana, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Ezekiel Kyunga alisema kuwa bado walikuwa hawajawafikia watu hao lakini wamefika chini sana na kukaribia njia hizo za Mlalo.
“Kinachofanyika sasa ni kuondoa udongo kwenye njia kwa kutumia watu kwa kufanya taratibu na kwa umakini mkubwa ili udongo usiporomoke tena katika eneo hilo,” alisema.
Alieleza kuwa matumaini yao ya kuwakuta watu hao wakiwa hai bado ni makubwa kwani uokoaji huo unafanyika kwa umakini lakini kwa haraka sana na sehermu iliyobaki kufikia njia hizo ni ndogo sana.
Watu hao akiwemo raia wa China mmoja walifukiwa na kifusi juzi usiku baada ya udongo kukatika na kuziba mlango waliokuwa wakitumia kuingia na kutoka na uokoaji unaendelea kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya uokoaji.
Kyunga alieleza kuwa watu wengi wapo katika eneo hilo wakiwemo ndugu wa waliofukiwa lakini kwa juhudi wanazoziona za uokoaji wametulia na kufuata maelekezo wanayopewa ikiwemo kukaa mita 500 toka eneo la tukio.
Alisema wametakiwa kukaa mbali na eneo hilo la uokoaji ili wasisongamane na watu wanaoendelea na uokoaji ili kuwapa fursa nzuri ya vikosi vyote kujadiliana namna ya kufanywa kwa ajili ya kufanikisha uokoaji huo.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni