Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Felix
Ngamlagosi akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo
juu ya ongezeko la bei ya umeme, Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Umeme,
Godfrey Chibulunje katikati Meneja Mawasialiano wa mamlaka hiyo Titus
Kaguo.
Mamlaka
ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeidhinisha asilimia
8.5 ya ongezeko la bei ya huduma za umeme ili kukidhi gharama za
uzalishaji wa umeme.
Ongezeko
hilo limetangazwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka
hiyo, Felix Ngamlagosi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
kuhusu maombi ya kurekebisha bei za umeme ambapo marekebisho hayo
yanatarajiwa kuanza kutekelezwa kuanzia Januari Mosi mwaka 2017.
Ngamlagosi
amesema kuwa TANESCO iliomba kuidhinishiwa ongezeko la bei ya huduma
hizo ili kuliwezesha shirika hilo kupata fedha za kulipia gharama za
uendeshaji, kupata fedha za uwekezaji katika miundombinu pamoja na
kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia asilimia 75 ya wananchi wote
ifikapo mwaka 2025.
”Baada ya
TANESCO kuwasilisha taarifa zinazohitajika kwa ajili ya kukamilisha
maombi yao, EWURA ilifanya mikutano ya taftishi, matangazo kwa umma
pamoja na kushirikisha wadau mbalimbali kutoa maoni juu ya ongezeko hilo
ambapo baada ya uchambuzi wa maoni hayo tulilidhia kuongeza asilimia
8.5 tu ya ongezeko la bei hizo ,” alisema Ngamlagosi.
Mkurugenzi
huyo ameongeza kuwa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) ambalo linanunua
umeme wa jumla kupeleka Zanzibar limeongezewa asilimia 5.7 ya bei ya
umeme badala ya asilimia 19.1 iliyoombwa na TANESCO.
Amefafanua
kuwa kulingana na marekebisho yaliyofanyika, jumla ya mapato
yanayohitajika kwa mwaka 2017 ni shilingi bilioni 1,608.47 ambayo ndiyo
iliyopelekea ongezeko la bei la wastani wa asilimia 8.5 hivyo gharama za
umeme zimeongezeka kutoka shilingi 242.34 kwa uniti moja hadi shilingi
263.02 kwa uniti moja.
Aidha,
Mkurugenzi huyo ametoa maagizo kwa TANESCO yakiwemo ya kuanzisha tozo ya
mwezi ya shilingi 5,520 kwa wateja wa kundi linalohusisha viwanda
vidogo, mabango na minara ya mawasiliano, kuboresha huduma kwa wateja
pamoja na kuacha kuwaunganisha wateja wadogo kwenye kundi la wateja
wakubwa na badala yake kuwaonganishe moja kwa moja katika kundi la
wateja wadogo.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni