KAMISHENI
ya Ngumi za Kulipwa nchini (TPBC) imemfungia Bondia Francis Cheka
kushiriki katika mchezo wa ngumi kwa kipindi cha miaka miwili na kulipa
faini ya shilingi laki tano kwa kitendo cha kukacha pambano baina yake
na Bondia Abdallah Pazi (Dulla Mbabe).
Akizungumza
na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Katibu Msaidizi wa
TPBC, Chatta Michael alisema kamisheni hiyo ilitoa kibali cha pambano
kati ya Cheka na Abdallah Pazi lakini bondia huyo hakufika katika
pambano hilo huku akiwa ameshalipwa kiasi cha shilingi milioni tatu.
Chatta
alisema kuwa Cheka aliaharisha pambano hilo lililokuwa lifanyike katika
ukumbi wa Sabasaba tarehe 25 Desemba mwaka huu pasipo na kutoa taarifa,
wakati Promota wa pambano hilo alikwishaingia gharama mbalimbali za
maandilizi ya pambano hilo.
“Kamisheni
imejiridhisha kuwa kiasi cha shilingi milioni tatu kilitolewa kwa
Francis Cheka kabla ya pambano, hivyo alitakiwa apatiwe kiasi
kilichobaki baada ya pambano kama alivyokubali na kusaini mkataba wa
pambano hilo,” alifafanua Chatta.
Aliongeza
kuwa kitendo cha kutotii makubaliano na kuchukua fedha bila kuifanyia
kazi si jambo la kawaida kwa kuwa lina madhara makubwa katika kuendeleza
mchezo wa ngumi za kulipwa nchini.
Kwa
mujibu wa Chatta alisema TPBC imetoa adhabu hiyo ili kuwa fundisho kwa
mabondia wengine ambao wanaweza kusababisha mchezo wa ngumi kupoteza
uaminifu kwa wakuzaji na kusababishha uvunjifu wa amani kwa watazamaji
iwapo wataendelea kudanganywa kuhusu uwepo wa mapambano hewa.
Kwa
upande wake, Rais wa TPBC,Chaurembo Palasa alisema adhabu hiyo ni mwanzo
wa kuboresha mchezo wa ngumi za kulipwa kwani mchezo huo umekuwa
ukiendeshwa bila kufuata sheria, kanuni na taratibu kwa muda mrefu.(P.T)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni