TAARIFA HUKUJUZA MENGI YA ULIMWENGUNI

Jumanne, 4 Oktoba 2016

WAUGUZI KUWASHTAKI WANASIASA KWA RAISI MAGUFULI

Hakuna maoni


CHAMA cha wauguzi Tanzania kinatarajia kufanya mkutano mkuu wake wa mwaka huu mjini Kigoma, ajenda kuu ni kupeleka kilio chao kwa Rais John Magufuli kuhusiana na matatizo yanayowakabili katika utendaji kazi wao, ikiwemo wanasiasa kuwahukumu.
Rais wa chama cha wauguzi nchini, Paul Magesa akizungumza na waandishi wa habari jana alisema mkutano huo unatarajia kuwakutanisha wauguzi zaidi ya 1,000 kutoka mikoa yote nchini na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalim anatarajia kuwa mgeni rasmi.
Alizitaja baadhi ya matatizo yanayowakabili ni wanasiasa kuwahukumu bila kufanya uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili na kutochukua hatua kulingana taratibu za utumishi.
Sambamba na hilo, alisema kuwa upande wa maslahi ya watumishi limekuwa tatizo kubwa ambapo pamoja na kuonana na Kamati ya bunge ya maendeleo ya jamii, bado hilo haijapatiwa ufumbuzi.
Rais huyo amesema hawana msimamizi mmoja wa matatizo yao ambapo kwa sasa yanashughulikiwa na wizara tatu ikiwemo Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais, utumishi na hapo hapo wakiwa chini ya usimamizi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za mikoa na serikali za mitaa (Tamisemi).
Kutokana na hali hiyo, kiongozi huyo alisema wanapaswa kuwekwa chini ya mwavuli mmoja ambao utakuwa unaangalia utendaji wao, kushughulikia stahiki zao mbalimbali na mambo ya nidhamu na maadili katika utendaji kazi wao.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni