TAARIFA HUKUJUZA MENGI YA ULIMWENGUNI

Jumanne, 4 Oktoba 2016

MVUA YALETA MADHARA

Hakuna maoni

NYUMBA zaidi ya 30 zimeharibiwa kwa mvua ya mawe iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha katika kijiji cha Kalalasi, wilayani Kalambo, mkoani Rukwa na kumjeruhi mkazi wa kijiji hicho huku familia kadhaa zikikosa makazi.
Majeruhi Agnes Isaack na amelazwa hospitalini mjini Matai kwa matibabu baada ya kujeruhiwa mwilini na bati lililopeperushwa hewa na upepo mkali baada ya kuezuliwa na mvua hiyo. Maafa hayo yametokea ikiwa ni wiki tatu tangu maafa mengine kutokea katika kijiji cha Mtimbwa, Manispaa ya Sumbawanga na kuharibu nyumba 12.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu akiwa kijijini humo, Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Matheo Ndeje, alisema mvua hiyo ilinyesha kwa saa mbili jana kuanzia saa 10:00 jioni na ilisababisha taharuki kubwa kijijini humo. Alisema vyoo vya Shule ya Msingi Kalalasi vimebomolewa huku upande mmoja wa paa la ghala la kijiji limeezuliwa.
“Tumepita maeneo mbalimbali ili kushuhudia athari iliyosababishwa na mvua hiyo na kubaini nyumba 32 zimeharibiwa huku nyumba 20 zimebomoka, nyingine kuta na nyingine paa zimeezuliwa. Vyoo vyote katika shule yetu ya msingi kijijini hapa imeezuliwa huku upande wa paa wa ghala la kijiji limeezuliwa,” alisisitiza.
Taarifa kutoka mjini Matai zinaeleza kuwa, Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Julieth Binjura akiongozana na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya wamefika kijijini humo.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando alisema hadi sasahakuna kifo chochote kilichoripotiwa.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni