RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein amesifu uhusiano uliopo kati ya Zanzibar na Cuba na kusisitiza dhamira ya Zanzibar kuendeleza uhusiano na ushirikiano huo.
Akizungumza na Makamu wa Rais wa Cuba, Salvador Antonio Veldes Mesa ambaye yuko nchini kwa ziara rasmi. Dk Shein alisema sasa ni wakati muafaka kuangalia maeneo mengine zaidi ya ushirikiano kwa manufaa ya wananchi wa pande zote.
Dk Shein alibainisha kuwa miaka 52 ya uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Cuba, imeshuhudia mafanikio makubwa ambayo yameridhisha pande zote.
Aidha alisema Zanzibar inajivunia uhusiano wake na Cuba kwa kuwa ni rafiki wa kweli na kuieleza hatua ya Cuba kuwa nchi ya kwanza kuitambua Zanzibar baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964 yaliyouondoa utawala wa kusultani, inathibitisha urafiki huo.
Chini ya ushirikiano huo, Dk Shein alisema Zanzibar imekuwa ikifaidika na misaada ya kimaendeleo ambayo ni chachu katika kuimarisha juhudi za serikali kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Dk Shein alitumia fursa hiyo kuishukuru serikali ya Cuba kwa kusaidia kuanzisha shule ya tiba kwa kushirikiana na Chuo kikuu cha Mathansas ambayo imeweza kutoa madaktari 38 ambao tayari wameajiriwa serikalini, huku wengine 14 wakitarajiwa kumaliza hivi karibuni baada ya shule hiyo kuhamishiwa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA).
Aidha, ameishukuru serikali hiyo kwa kuridhia ombi la Zanzibar la kuwatumia walimu madaktari wa Chuo Kikuu cha Mathansas kubaki kufundisha katika Shule ya Sayansi za Afya na Tiba ya SUZA, hatua ambayo itaimarisha chuo hicho.
Aidha, Dk Shein alimueleza Makamu wa Rais huyo wa Cuba kuwa yako maeneo mengi ambayo Cuba na Tanzania zinaweza kushirikiana ikiwemo uvuvi, viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, utalii, biashara na uwekezaji katika nyanja mbalimbali.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Cuba, Salvador Antonio Veldes Mesa alieleza kuwa ziara yake hii inalenga katika kuimarisha na kuendeleza uhusiano wake na Tanzania.
Alisema amefurahi kuwa ziara hiyo imemfikisha Zanzibar mahala ambapo ni moja ya mfano wa mafanikio wa ushirikiano wa wananchi wa Cuba na nchi za nje katika masuala ya afya.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni