CHAMA cha Kuogelea Tanzania (TSA) kinatarajia kufanya mkutano wa marekebisho ya katiba Ijumaa visiwani Zanzibar ikiwa ni siku moja kabla ya kufanyika kwa mashindano ya kuogelea ya taifa.
Katibu Mkuu wa TSA, Ramadhan Namkoveka alisema kuwa mkutano huo wa katiba utafanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Baraza la Michezo la Zanzibar kuanzia asubuhi.
“Kwa muda mrefu tumekuwa katika mchakato wa kufanyia marekebisho ya katiba kwa njia ya kupokea maoni baada ya TSA kuandaa rasimu na kupelekwa kwa wanachama wetu ambao ni klabu,” alisema.
Alitolea ufafanuzi hoja ya kufanya marekebisho kuwa imetokana na sababu mbalimbali, ikiwemo hali iliyojitokeza katika uchaguzi mkuu wa chama (TSA) uliofanyika Morogoro Oktoba 10, 2015 ambapo Chama cha Kuogelea Zanzibar na chama cha makocha (TSCA) hawakupiga kura kwa kuwa katiba ilikuwa haiwatambui.
Pia, alisema kamisheni ya wachezaji ni lazima wawepo kwenye kamati ya utendaji, vyeo kama Mkurugenzi wa Ufundi, Mkurugenzi wa Fedha na vinginevyo havijatajwa moja kwa moja kwenye katiba.
“Kutokana na sababu hizo ni lazima katiba yetu ifanyiwe marekebisho yanayostahili ili iendane na wakati uliopo na kwa maslahi ya chama na mchezo wa kuogelea kwa ujumla,” alisema.
Alisema watu wengine walioshiriki kutoa maoni yao ni Kamati ya utendaji ya TSA na mwanasheria wao ambaye amefanya kazi kubwa kuhakikisha sheria za Shirikisho la Kuogelea Duniani (FINA) na za nchi zinazingatiwa.
Namkoveka alisema juhudi za mchakato huo zitaishia siku hiyo kwa kupitisha marekebisho yaliyopendekezwa kama itapata ridhaa kutoka kwa wajumbe wa mkutano wa katiba watakaohudhuria na kupelekwa kwa msajili wa vyama vya michezo ili kupata ridhaa ya serikali.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni