TAARIFA HUKUJUZA MENGI YA ULIMWENGUNI

Jumatatu, 3 Oktoba 2016

FUNGASHENI BIDHAA KWA VIPIMO VYA KIMATAIFA

Hakuna maoni
WAKALA wa Vipimo (WMA), imewataka wafanyabiashara kuhakikisha wanafungasha bidhaa zao kwa kutumia vipimo vya kimataifa vinginevyo wataharibu soko la bidhaa za Tanzania nje ya nchi.
Aidha, wakala huo, umeanza kufanya ukaguzi katika maeneo ya mipakani, viwandani na Bandari ya Dar es Salaam ili kuhakikisha bidhaa zimefungashwa katika viwango vya kimataifa.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ufundi wa Mamlaka hiyo, Stella Kahwa, alisema, kila mfanyabiashara nchini ana wajibu wa kuhakikisha anafuata vipimo hivyo vya kimataifa, ili kumlinda mlaji, lakini pia kulijenga soko la nchi nje ya nchi.
Alisema kwa sasa, WMA inafanya ukaguzi katika mipaka ya Horiri, Sirari na Namanga na pia inafanya ukaguzi kwenye Bandari ya Dar es Salaam ili kuendeleza jukumu hilo na kuilinda Tanzania isiwe sehemu ya kuingiza bidhaa zisizozingatia sheria ya vipimo.
Pia, alieleza kuwa umuhimu wa kuhakiki bidhaa zilizofungashwa kuwa ni pamoja na kumlinda mlaji na kuhakikisha kuwa biashara zote zinafanyika kwa haki na usawa baina ya pande mbili zinazohusika muuzaji na mnunuzi kupitia vipimo.
Alisema vipimo sahihi humwezesha mnunuzi kununua bidhaa hiyo kulingana na thamani ya fedha yake. Alieleza kuwa uhakiki wa bidhaa zilizofungashwa unasaidia kudhibiti kiasi sahihi katika ufungashaji wa bidhaa hizo, hivyo kuiwezesha Serikali kutoza kodi sahihi.
Mkuu wa Kitengo cha Sheria kutoka Wakala wa Vipimo, Mosses Mbunda, alisema atakayebainika amekiuka kanuni za bidhaa zilizofungashwa, ataadhibiwa kama sheria inavyosema, chini ya kifungu cha 45 cha Sheria ya Vipimo Sura 340 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Alisema kwa mujibu wa sheria hiyo, mkosaji wa mara ya kwanza adhabu yake ni faini isiyozidi Sh 10,000 au kifungo cha miaka mitatu jela, au vyote na kwa mkosaji wa mara ya pili faini isiyozidi Sh 20,000 au kifungo cha miaka saba au vyote kwa pamoja

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni