WABUNGE wanawake kutoka Kambi ya Upinzani inayoundwa na vyama
vilivyoko katika kundi la Ukawa, jana walitoka nje ya Bunge baada ya
kukerwa na neno ‘bebi’, lililotumiwa juzi na Mbunge wa Ulanga Mashariki
Goodluck Mlinga (CCM).
Mlinga alichafua hali ya hewa ndani ya Bunge juzi jioni, wakati
akichangia katika Ba ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2016/2017,
baada ya kusema wanawake waliopata ubunge kutoka Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), wamepata nafasi hiyo baada ya kuitwa ‘bebi’.
“Kila mwanamke ndani ya Chadema kaingia ubunge kwa sifa yake lakini
sifa kubwa ni lazima uitwe bebi. Chadema kuna wanachama wengi wa kike
iweje ichukue wa CCM. Chadema ndiyo inakandamiza demokrasia, Tundu Lissu
anajua sheria lakini ndani ya Chadema kuna wapenzi wa jinsia moja,”
alisema.
Baada ya kutoa kauli hiyo majira ya saa 11:39 jioni, hali ilibadilika
ndani ya Bunge, walisimama wabunge wote wa Chadema na CUF wakiomba
utaratibu na kupiga kelele za kuonesha kukerwa na kauli hiyo.
Waliendelea kupiga kelele licha ya Naibu Spika, Dk Tulia Ackson
kuwataka watulie na hali hiyo iliendelea kwa takriban dakika nne na
kumfanya Naibu Spika kumuomba Mnadhimu wa Bunge wa Kambi ya Upinzani,
Lissu awatulize upande wa upinzani.
“Naomba mtulie, naomba mtulie, Lissu watulize watu wako ili
tuendelee,”alisema na baada ya sekunde chache wabunge wote walikaa chini
na Lissu akasimama na kuzungumza.
Kauli ya Lissu
Lissu alisema “Kanuni ya 64 inakataza mbunge kumsema vibaya mbunge
mwingine au kumdhalilisha mtu mwingine, mjumbe aliyemaliza kuzungumza
(Mlinga) katoa maneno ya udhalilishaji kwa wanawake na kukiuka kanuni za
Bunge. “Kama msemaji anabisha hoja basi abishie hoja lakini amesema
mambo ya nje ya Bunge, amezungumzia mahusiano binafsi, naomba kiti chako
kichukue hatua stahiki ili lugha ya kudhalilisha wanawake ikome,”
alisema Lissu.
Naibu Spika Baada ya Lissu kumaliza, alisimama Naibu Spika na kusema
“Lissu ametukumbusha mambo yasiyoruhusiwa, lugha zinazotumika humu pande
zote mbili haziko sahihi, tutumie lugha za kibunge, kuita wengine
wajinga au tabia za watu fulani hazifai. Goodluck endelea kwa lugha
nzuri”.
Hata hivyo Goodluck alishindwa kuendelea licha ya kupewa nafasi
kutokana na wabunge wa upinzani kusimama na kupiga kelele wakimtaka
afute kauli yake.
Kitendo hicho kilimfanya tena Naibu Spika kusimama na kuwataka wakae
chini kisha akampa nafasi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,
Bunge, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama.
*Mhagama
Mhagama alisema; “alichosema Naibu Spika ni sawa, pande zote mbili
kumetolewa lugha zisizofaa, sisi mawaziri tumetukanwa tukiambiwa
wajinga, kuna mtu kaitwa kigodoro humu, si haki kuruhusu upande mmoja
utukanwe, Naibu Spika tumia kiti kufuta maneno yote ya matusi ya leo,”
alisema.
Naibu Spika akasema “naagiza maneno ya udhalilishaji kwa CCM na
upinzani yafutwe,” ndipo akaruhusiwa Goodluck kuendelea naye akafuta
kauli yake.
Waamka nayo
Jana Mbunge wa Viti Maalumu Sophia Mwakagenda (Chadema), aliomba
mwongozo wa Spika kutokana na kauli ya juzi ya Mlinga na aliporuhusiwa,
alisema kauli hiyo ni ya udhalilishaji si kwa wabunge wanawake wa
upinzani, bali kwa wanasiasa wote wanawake na haipaswi kupigiwa makofi.
“Hata Rais wetu aliyepita (Jakaya Kikwete) alitambua umuhimu wa kutoa
nafasi kwa wanawake na ndio maana uteuzi wake ulizingatia usawa. “Sasa
imenishangaza hapa bungeni pamoja na mbunge huyu kutoa kauli za
udhalilishaji dhidi ya wanawake, wapo wanawake wenzetu wanashangilia na
tena na kupiga makofi,” alisema Mwakagenda.
Alisema akiwa mwanamke mwanasiasa hataki kuamini kama wanawake wote
waliomo ndani ya siasa, wamepitia kwanza kwenye mchakato wa uzinifu
ndipo wakafanikiwa kupata nafasi za uongozi.
Alisema kutokana na kitendo cha Chama cha Wanawake Wabunge kutochukua
hatua zozote dhidi ya kauli hiyo iliyodhalilisha wanawake, anajivua
rasmi uanachama wa chama hicho.
Dk Ackson wakati akijibu mwongozo huo, alisema tayari alishatolea
mwongozo kauli hiyo tangu katika mjadala wa juzi jioni wa kupitisha
makadirio ya matumizi na mapato ya Wizara ya Katiba na Sheria.
“Nilisema kuwa pande zote mbili zilitumia maneno mabaya na kuagiza
kauli hizo zifutwe kwenye taarifa za Bunge. Kwa maana hiyo naomba
tuendelee na ratiba,” alisema Naibu Spika.
Vurugu
Baada ya kauli yake hiyo wabunge hao wanawake wa upinzani
hawakukubali, wakaamua kusimama huku wengi wao wakiomba taarifa na
miongozo ingawa hawakupatiwa nafasi.
Mara baada ya Dk Ackson kumaliza kutambulisha wageni waliofika
bungeni hapo, vurugu ziliibuka tena bungeni hapo, ambapo wanawake wote
wa upinzani walisimama huku wakipinga Bunge kuendelea bila mwongozo huo
kujibiwa.
“Nawaomba mkae, suala hili silizungumzii tena nimeshalipatia majibu.
Waheshimiwa kaeni chini, nasema kaeni chini,” alisema Naibu Spika kauli
ambayo hata hivyo wabunge hao hawakuitii.
Wakati hali ya sintofahamu ikiendelea bungeni hapo, baadhi ya wabunge
wa upinzani walisikika wakirusha maneno ya kejeli dhidi ya Naibu Spika
huku wakidai kuwa wao si wanafunzi na kiongozi huyo wa Bunge si mkuu wa
shule.
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) alisikika akisema;
“msituburuze, usitumie kiti vibaya tuna haki kwa mujibu wa sheria,
tunaomba kupewa nafasi ya mwongozo hatuwezi kuvumilia udhalilishaji
huu.”
Dk Ackson aliyekuwa pia amesimama aliwafokea wabunge hao kwa kuvunja
kanuni inayowataka wakae chini wakati yeye amesimama. “Waheshimiwa kaeni
chini, nasema mliosimama kaeni chini, nimesema kaeni chini, ninawaomba
kwa mara ya kwanza jamani kaeni chini tuendelee.”
Watolewa nje
Baada ya jaribio la kuendelea na ratiba kushindikana kutokana na
kelele za wabunge hao, Dk Ackson alilazimika kuwaagiza wabunge hao
watoke nje, agizo ambalo walijaribu kukaidi hadi pale askari wa Bunge
takriban watatu walipowasili.
Wakati wakiondoka ndani ya Bunge hilo, wabunge hao akiwemo Mdee na
Esther Bulaya (Chadema), pamoja na baadhi ya wabunge wa upinzani
walitupa hewani vitabu vya Bunge vilivyokuwa kwenye meza zao za shughuli
za Bunge kwa siku hiyo.
Baada ya wabunge hao kutoka nje huku wakifuatwa nyuma na mbunge wa
Urambo Mashariki ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho cha TPWG Margaret
Sitta, mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema),
aliendelea kuomba mwongozo lakini Dk Ackson alimkatalia.
“Acha kutuburuza bwana,” alisema Msigwa huku akiwa amekasirika na
kuchukua vifaa vyake na kutoka nje. Wakiwa nje wa ukumbi wa Bunge, Mdee
aliyezungumza kwa niaba ya wabunge wenzake wanawake wa Ukawa, alisema
Naibu Spika amevunja Katiba kwa kukataa kuwaruhusu watoe miongozo yao
kwa mujibu wa Kanuni za Bunge.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni