SAKATA la kupanda kwa bei ya sukari limeibuka tena bungeni na safari
hii Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) ameomba mwongozo wa
kutaka Kikao cha Bunge kiahirishwe ili kujadili suala hilo la dharura.
Akitumia kifungu cha Kanuni za Bunge cha 47(1, 2, 3), mbunge huyo
alisema bungeni mjini hapa jana, kuwa suala hilo ni muhimu kwa
Watanzania hivyo ni vyema likajadiliwa na kupatiwa ufumbuzi haraka
iwezekanavyo.
Alisema tangu itangazwe utaratibu wa kusitisha sukari kuingizwa
nchini kutoka nje, bidhaa hiyo imekuwa adimu na bei yake imekuwa
inapanda kila siku na kusababisha maisha ya wananchi kuzidi kuwa magumu.
Hata hivyo, kabla ya kumaliza kuwasilisha hoja yake hiyo, Naibu Spika
wa Bunge, Dk Tulia Ackson alimkatisha na kubainisha kuwa hoja hiyo si
dharura, lakini pia tayari ilishatolewa ufafanuzi na Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa.
Wiki iliyopita, Waziri Mkuu akijibu hoja iliyoibuliwa bungeni hapo
inayohusu pia bei ya sukari, Waziri Mkuu alisema serikali imeruhusu
kiasi kidogo cha sukari kuingizwa nchini ili kupunguza tatizo la
upungufu wa bidhaa hiyo.
Kwa mujibu wa Majaliwa, Tanzania ina uwezo wa kuzalisha tani 300,000
za sukari kwa mwaka wakati nchi inahitaji tani 420,000 hivyo kuwepo na
upungufu wa tani 120,000.
Aidha, mapema mwezi uliopita, serikali ilitangaza kuwa bei elekezi ya
sukari itakuwa Sh 1,800 kwa kilo, lakini hali katika maeneo mbalimbali
nchini ni tofauti, kwani bidhaa hiyo muhimu inauzwa kwa bei ya juu.
Katika maeneo mbalimbali ukiwamo Mkoa wa Dar es Salaam, sukari
inauzwa kuanzia Sh 2,200 hadi Sh 2,500 kwa kilo, wakati baadhi ya mikoa
ikiwamo Kagera ambako inazalishwa katika Kiwanda cha Kagera kilichopo
Missenyi, bei inatajwa kufikia hadi Sh 25,000 kwa kilo moja.
Baadhi ya wafanyabiashara nchini wameamua kufanya njama za kuficha
bidhaa hiyo ili kuonekana kuwa kuna uhaba ili waruhusiwe kuagiza kutoka
nje, jambo ambalo limekwishakataliwa na Rais John Magufuli.
Wiki iliyopita, mkoani Singida, wananchi walisaidia kukamatwa kwa
mifuko 655 ya sukari sawa na tani 24.3, na kutiwa nguvuni
wafanyabiashara wawili pia wakihusishwa na bidhaa hiyo ambayo ilifichwa
stoo.
Waliokamatwa ni Mohamed Alute Ally (44) mfanyabiashara wa Unyankindi
aliyekutwa na mifuko 335 ya kilo 25 kila mmoja na Yusufu Suleiman (39)
mfanyabiashara wa Minga aliyepatikana na mifuko 320 ya kilo 50.
Taarifa ya kukamatwa kwa sukari hiyo na wafanyabiashara hao ilitolewa
na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ambaye pia ni
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Saidi Amanzi.
Taarifa zilieleza kuwa mfuko mmoja wa sukari ambao huuzwa kwa Sh
92,650 sasa unauzwa kati ya Sh 115,000 na Sh 120,000 huku kilo moja
ikiuzwa kati ya Sh 2,400 na 2,800 kwa kilo kinyume cha bei elekezi ya Sh
1,800.
Gazeti hili lilifanya jitihada za kuwasiliana na Mkurugenzi Mkuu wa
Bodi ya Sukari Tanzania, Henry Simwanza kuzungumzia hali ya bei hiyo
jana, lakini awali alipopigiwa simu alieleza kuwa yuko bungeni, lakini
baadaye hakupokea simu ya gazeti hili kutwa nzima alipotafutwa.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni