SAKATA la ufichaji sukari lililoanzishwa na wafanyabiashara wasio
waaminifu nchini, limechukua sura mpya baada ya Rais John Magufuli
kutaja baadhi ya maeneo sukari hiyo ilikofichwa na kuagiza ikamatwe,
itaifishwe na kugawiwa bure kwa wananchi.
Kwa sasa sukari imeshaanza kuadimika, ambapo katika maduka ambayo
ilikuwa kawaida kukuta bidhaa hiyo katika makazi ya wananchi,
haipatikani kabisa na inakopatikana, bei yake iko juu maradufu zaidi ya
bei elekezi ya Sh 1,800 kwa kilo.
Takwimu za bei zimekuwa zikibadilikabadilika katika maeneo ya Dar es
Salaam ambako wiki hii ilishafikia Sh 2,500 huku mikoani ikiongezeka na
kuzidi Sh 3,000.
Walioficha Dar, Moro
Akizungumza jana na wananchi katika mji wa Katesh wilayani Hanang
mkoani Manyara akiwa njiani kwenda mkoani Arusha, Rais Magufuli alisema
taarifa alizokuwa nazo mpaka jana kuna baadhi ya wafanyabiashara
wameficha sukari tani 7,000.
“Kuna mmoja alienda kununua sukari Kilombero (mkoani Morogoro) zaidi
ya tani 3,000 na kuiacha iko pale pale na mwingine ana godown (ghala)
Mbagala (jijini Dar es Salaam), akiwa na tani 4,000 na hataki kuitoa ili
wananchi wakose sukari, lakini nataka kuwaambia sukari huwezi kuficha
kama sindano,” alisema huku akitoa mifano.
“Tutachukua sukari ile na kugawa bure na hawatafanya biashara
maishani hapa nchini Tanzania, hivyo kama wapo wafanyabiashara
wanaonisikia ambao wanataka kucheza na Serikali hii wanacheza na maisha
yao,” alionya Rais Magufuli, ambaye uongozi wake umejivunia sifa ya
kuchukua maamuzi ya kijasiri.
Kiwango hicho cha sukari iliyofichwa katika maghala mawili tu ya
Morogoro na Dar es Salaam, kinatosheleza kulisha nchi nzima kwa wiki
moja, kwa kuwa mahitaji ya siku ya sukari nchini ni tani 1,150 sawa na
tani 420,000 kwa mwaka.
Salama la ambao hawajagundulika kwa mujibu wa Rais Magufuli, ni kutoa
sukari waliyoficha kwa wananchi na kuiuza kadri walivyokuwa wamepanga.
Kwa watakaokaidi, Rais Magufuli ameagiza vyombo vya dola kufuatilia
wafanyabiasha wote walioficha sukari, kwani ni wahujumu uchumi na sukari
waliyoficha itachukuliwa na kugawiwa bure.
Sababu ya kudhibiti
Akielezea sababu za kuzuia uagizaji wa sukari nje ya nchi, Rais
Magufuli alisema wakulima nchini wanalima miwa, lakini haitengenezi
sukari kwa kuwa kuna sukari ya magendo inayoingizwa kutoka nje ya nchi.
Mbali na kuwa ya magendo, Rais Magufuli alisema wafanyabiashara hao
wanaoingiza sukari ya magendo, wana tabia ya ajabu kwenda nchini Brazil
na maeneo mengine kunakouzwa sukari inayokaribia kuisha muda wake wa
matumizi na kutaka kutupwa na kuinunua wao.
Alisema sukari hiyo ambayo katika nchi husika hutakiwa kumwagwa
baharini, wafanyabiashara wenye tamaa ya fedha wa hapa nchini, huichukua
na kuweka kwenye magunia tofauti na kuileta ndiyo maana wananchi
wanapata magonjwa ya kila aina ambayo haijulikani yametoka wapi.
“Tunataka kudhibiti biashara hii ya sukari kwani tatizo ni dogo
niwaambie ni la muda, kwani Serikali ya Magufuli haiwezi kushindwa
kununua sukari hata kama ni mabehewa elfu ngapi,” alisema. Alisema
ameshamuagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na sukari ya kutosha italetwa
na watu watapata bei ya sukari iliyo nafuu.
*Uagizaji kukomeshwa
Pamoja na uhaba uliopo ambao kwa sehemu kubwa umetengenezwa na
wafanyabiashara hao baada ya kuzuiwa kuagiza sukari kutoka nje, tayari
Serikali imeshachukua hatua za uzalishaji zaidi, zitakazokomesha kabisa
biashara ya uagizaji wa sukari kutoka nje ya nchi.
Wiki iliyopita wakati Waziri Mkuu Majaliwa akijibu maswali ya papo
kwa hapo bungeni kuhusu pia bei ya sukari, alisema Tanzania ina uwezo wa
kuzalisha tani 300,000 za sukari kwa mwaka wakati mahitaji ya bidhaa
hiyo kwa mwaka ni tani 420,000 na hivyo upungufu kuwa tani 120,000 kila
mwaka.
Jana Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage,
alielezea hatua hizo za kukomesha uagizaji wa sukari, wakati akijibu
swali la nyongeza la Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilango (CCM), aliyetaka
kufahamu lini Mkoa wa Kigoma wenye rasilimali nyingi kutajengwa viwanda.
Kwa mujibu wa Mwijage, kiwanda kipya cha sukari kinatarajiwa kujengwa
katika mkoa huo na tayari Serikali imeshampa mwekezaji wa kiwanda
hicho, hekta za ardhi 47,000 kwa ajili ya mradi huo.
Mwijage alisema kiwanda hicho kitakapoanza uzalishaji, kitazalisha
tani 120,000 za sukari kwa mwaka, ambazo ndizo zinazopungua katika
uzalishaji wa sasa.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni