Rais John Magufuli ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kutowachagulia vyuo wanafunzi wa elimu ya juu na kuwaacha wanafunzi hao kuchagua vyuo wanavyovitaka wenyewe.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Rais Magufuli alipokuwa akizindua mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambapo alikitaka chuo hicho pia kutoza Sh 500 kwa siku tofauti na Sh 800 ambazo zinatoswa kwa hosteli nyingine.
“Ninaamini kama wanafunzi wangepewa nafasi ya kuchagua vyuo wanavyovipenda wenyewe, vyuo vya Serikali kama vile Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo Kikuu cha Mzumbe vingekuwa na wanafunzi wengi sana,” alisema Magufuli.
Aliendelea kwa kusema kuwa TCU imekuwa ikiwachagulia wanafunzi vyuo visivyo na sifa na makazi ya wanafunzi hivyo kusababisha wanafunzi hao kusoma katika mazingira magumu na wanapomaliza masomo yao hukosa ajira kutokana na vyuo hivyo kutokuwa na sifa. Rais Magufuli alitaka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) lenyewe kubaki na udhibiti.
Aidha alisema ni vyema Tume ikabaki na majukumu yake kama kuhimiza ubadilishaji wa maarifa/elimu kwa njia ya kuunganisha kimtandao Vyuo Vikuu na Vyuo vya Vyuo Vikuu, usajili na utambuzi rasmi wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Vyuo Vikuu, uthibitishaji wa programu za kitaaluma, uthibitishaji na uratibu wa udahili wa wanafunzi.
Majukumu mengine ni ufuatiliaji na udhibiti wa elimu bora Vyuo Vikuu na Vyuo vya Vyuo Vikuu, ukusanyaji na usambazaji wa taarifa/ data kuhusu elimu ya juu. “Niombe tu kwa Wizara ya Elimu na TCU tubadilishe kidogo utaratibu wa kuchagulia wanafunzi, wanafunzi wawe wanachagua vyuo badala ya TCU kuwachagulia vyuo vya kwenda,” alisema. Akifafanua zaidi alisema kama wanafunzi wakijichaguliwa vyuo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kingejaa wanafunzi 23,000 wanaotakiwa kuwepo katika chuo hicho.
“Lakini sijajua ni kwa nini mtu amefaulu anataka kuja hapa afaidi mabweni ya Magufuli analazimishwa kwenda kwenye kachuo ambako hakana jina akasome pale, wakati hakuna hata mabweni, saa nyingine hata walimu hawana, tunawatesa watoto hawa,” alisema. Alisema anafahamu ingawa hana ushahidi kuwa wakuu wa vyuo hivyo wanatoa fedha kwa viongozi wa TCU ili wapangiwe idadi ya wanafunzi wanaowahitaji kwenye vyuo vyao.
Rais Magufuli alisema kuwa TCU ibaki kuwa mdhibiti wa elimu lakini wanafunzi wabaki kuwa na haki ya kuchagua vyuo kwani baadhi ya vyuo vinaendesha shughuli zake kwa mikopo ya wanafunzi hao. “Tuwaache watoto wachague vyuo wanavyovitaka, vile ambavyo havitachaguliwa, vife kwanini mnalazimisha vyuo ambavyo havina ubora vipate wanafunzi msipolazimisha vyuo ambavyo vina ubora vitapata watu….. najua maneno haya hayawafurahishi baadhi ya watu na mimi siko hapa kumfurahisha mtu?” alisema Rais Magufuli.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni