Baada ya sekeseke la kupiga marufuku uuzaji na unywaji wa
pombe kali viroba, wanywaji wa pombe za viroba mjini Dodoma wamebuni
mbinu mpya ya kununua pombe hiyo iliyopigwa marufuku huku watumiaji hao
wakiipa pombe hiyo jina la maziwa mgando au nzela.
Maeneo yanakopatikana viroba kwa wingi katika mji huo ni stendi ya
Mkoa wa Dodoma na Jamatini ambapo wafanyabiashara humimina pombe hiyo
katika chupa za konyagi.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti la Mtanzania kwa
siku kadhaa mjini hapo, umeonyesha jinsi pombe hiyo inavyouzwa kwa
shilingi 1,000 baada ya kujazwa kwenye chupa kubwa za konyagi.
Mmoja wa wauzaji wa pombe hiyo ambaye hakutaka kuandikwa jina lake
gazetini, alisema biashara imekuwa ngumu na wao wanahitaji kupata fedha,
hivyo wameamua kuja na njia mpya ya kuuza viroba hivyo. “Tutafanyaje
ndugu yangu, maisha magumu, tumeweka viroba katika chupa kubwa za
konyagi na tunawapimia kwa kutumia kakikombe kadogo kama ka kahawa kwa
shilingi 1,000,” alisema mfanyabiashara huyo.
Aliongeza”Siwezi kuacha hii biashara, hapa ni stendi, wasafiri na
makondakta wengi ndio wateja wetu na natengeneza fedha za kutosha,
lakini sasa hivi nawauzia tu watu ninaowajua, kwani naogopa kukamatwa.”
Naye mmoja wa wanunuzi wa viroba hivyo, alisema baada ya Serikali
kupiga marufuku uuzwaji wa viroba hivyo, wameamua kubadili mwelekeo wa
kununua bidhaa hiyo ili kukwepa mkono wa Serikali.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni