TAARIFA HUKUJUZA MENGI YA ULIMWENGUNI

Jumanne, 25 Oktoba 2016

WAJAZAWAZITO WANNE KULALA KITANDA KIMOJA

Hakuna maoni




MKUU wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri ametembelea wodi ya wazazi katika Hospitali ya Rufaa ya Kitete, mkoani Tabora, na kukuta wajawazito na wazazi waliojifungua, wakilala watatu au wanne katika kitanda kimoja.
Mwanri amesema, wajawazito na wazazi kulala mzungu wa nne au wa tatu, ni hatari kwa afya ya mama na mtoto.
Amemwagiza Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Nasoro Kaponta, kwa kushirikiana na uongozi wa hospitali hiyo, kufanya kila liwezekanalo ili kutatua changamoto hiyo, kwa kuwa ni hatari kwa afya ya mama na mtoto.
Ameuagiza uongozi wa hospitali hiyo, kuhakikisha wajawazito wanaoenda kujifungua hospitalini hapo, hawadaiwi fedha za vifaa vya kujifungulia, kwa kuwa serikali ilishaagiza wasitozwe gharama yoyote.
Dk Kaponta amemweleza Mwanri kuwa, msongamano huo unatokana na ufinyu wa nafasi katika wodi hiyo, ndio maana wanashindwa kuongeza vitanda na kuongeza kuwa, uchache wa zahanati na hospitali za wilaya pia unachangia kero hiyo.
Msimamizi wa huduma za akinamama katika wodi hiyo, Eliwampuka Mbwana, alisema kuwa kwa wastani wajawazito 25 hadi 30 wanakwenda hospitalini hapo kujifungua kila siku kutokana na ukosefu wa hospitali za wilaya na ndio maana kuna msongamano huo.
Ili kupunguza msonganano huo, mhudumu wa wodi hiyo, Eva Isaya alishauri zahanati na vituo vya afya vilivyopo katika Manispaa ya Tabora, vitumike kujifungulia na Hospitali ya Kitete ihudumie wale watakaopewa rufaa pekee.
Katika ziara hiyo Mwanri alikabidhi mashuka 38 ya Sh 500,000 katika wodi hiyo yaliyotolewa na wanafunzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Tawi la Tabora ambapo pia walitoa msaada wa chakula, mavazi na vitu vingine vyote vikiwa na thamani ya Sh milioni 1.5 kwa Kituo cha kulea Wazee kilichoko Ipuli.
Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Queen Mlozi alipongeza uongozi na wanafunzi wa chuo hicho kwa moyo wao wa kizalendo wa kuunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali katika kusaidia jamii kwa kuwa serikali pekee haiwezi kufanya kila kitu.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni