TAARIFA HUKUJUZA MENGI YA ULIMWENGUNI

Jumanne, 25 Oktoba 2016

TRAFIKI WASHTAKIWA KUTOZA FAINI BILA RISITI

Hakuna maoni

POLISI wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Arusha, wameshitakiwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kuwa wanatoza faini bila ya kutoa risiti kama Rais John Magufuli alivyoelekeza.
Mashitaka hayo yalisemwa na wafanyabiashara wakubwa walipokuwa na kikao na Gambo kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa mjini Arusha hivi karibuni kilichokuwa na lengo namna ya kushirikiana na serikali katika kufanya kazi za maendeleo.
Mfanyabiashara Sanjet Pandit anayemiliki Kampuni ya kitalii ya Roy Safari, amesema huwezi kulipa faini barabarani halafu unaambiwa risiti ukafuate Makao Makuu ya Trafiki.
Pandit amesema mbali ya hilo, kuna utitiri wa trafiki barabarani na siku nzima, dereva unaweza kusimamishwa zaidi ya mara sita, hali inayofanya kuwepo kwa usumbufu mkubwa.
Amemwomba Mkuu wa Mkoa kuwasiliana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Charles Mkumbo kuangalia namna ya utendaji kazi mzuri kati ya trafiki na wafanyabiashara.
Mustapher Panju anayemiliki Kampuni ya utalii ya Bushbark Safari, ametaka trafiki hao kutumia risiti za mashine za kielektroniki ili serikali ipate mapato na si vinginevyo.
Panju amesema utaratibu uliopo sasa wa kutozwa faini Njiro au Unga Ltd na kutakiwa kwenda kuchukua risiti halali ya karatasi Trafiki Makao Makuu si sahihi.
Amesema ni wakati wa trafiki hao kutumia risiti za EFDs ili kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli za kukusanya kodi halali ya serikali bila ya kuingia mikono michafu.
Mkuu wa Mkoa amemwagiza Kamanda wa Polisi, Mkumbo kufanyia kazi madai hayo haraka iwezekanavyo ili wenye kutozwa faini walipe faini halali kwa mujibu wa sheria.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni