TAARIFA HUKUJUZA MENGI YA ULIMWENGUNI

Jumatatu, 3 Oktoba 2016

LAPF KUPANUAUWEKEZAJI VIWANDA

Hakuna maoni
MFUKO wa Pesheni wa LAPF, umesema utashirikiana na wawekezaji na serikali kupanua wigo wa uwekezaji kwenye sekta ya viwanda ili kutoa fursa ya ajira na kuongeza wanachama wa mfuko huo kwa lengo la kukuza pato la taifa kiuchumi.
Mkurugenzi wa Huduma kwa Wanachama LAPF, Valerian Mablangeti, alisema hayo wakati wa kongamano la uwekezaji la mkoa wa Morogoro lililofanyika kwa siku mbili Septemba 29-30, mwaka huu mkoani hapa.
Alisema, uwekezaji katika sekta ya viwanda, utauwezesha mfuko kuongeza idadi ya wafanyakazi watakaojiunga na kujenga mfuko imara utakaotoa mafao bora zaidi kwa wanachama wake.
Mablangeti, alisema shughuli za uwekezaji katika mfuko zinafanywa kwa mujibu wa sera ya uwekezaji na miongozo mbalimbali ikiwamo ile ya Benki Kuu ya Tanzania pamoja na Mamkala ya Udhibiti na Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA).
Alisema miongozo hiyo, huelekeza maeneo ya uwekezaji, viwango vya faida katika eneo la uwekezaji na kiasi cha kuwekeza kwa kuzingatia mpango wa uwekezaji na ukizingatia dhima na wajibu wa muda mfupi na mrefu wa mfuko.
Mkurugenzi wa Huduma kwa Wanachama LAPF, alisema mfuko upo katika mazungumzo na Kampuni ya Ngulu Hill kwa ajili ya mradi wa kiwanda cha kutengeneza nyama ya ng'ombe na mbuzi.
Alisema, mradi mwingine ni wa kiwanda cha kuchakata chai kilichopo wilaya ya Lushoto, mkoani Tanga, pamoja na mradi wa kiwanda cha kutengeneza bandeji za hospitali kwa kutumia malighafi ya pamba mkoani Shinyanga.
Mablangeti , alisema uwekezaji mwingine ni wa ujenzi wa stendi ya mabasi Msamvu katika Manispaa ya Morogoro ambayo hadi kukamilika utagharimu Sh bilioni 9.7 na kwa sasa umefikia hatua za mwisho kabla ya kuzinduliwa rasmi.
"Mradi huu umeanza kutoa mafunzo ambapo makusanyo ya stendi yameongezeka kutoka Sh 90,000 kwa siku hadi milioni 1.5, " alisema Mablangeti .
Pamoja na hayo alisema , utaratibu umeandaliwa kwa kutenga maeneo ya maengesho na mabasi, taksi na pikipiki za usafirishaji ' bodaboda'.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni