KIPINDUPINDU kimeibuka upya katika Manispaa ya Dodoma na tayari wagonjwa 17 wameripotiwa kulazwa katika Hospitali ya Mirembe.
Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk James Charles, ugonjwa huo umeanza Septemba 28, mwaka huu ambako mgonjwa mmoja wa akili katika hospitali hiyo aligundulika kuugua kipindupindu.
Dk Charles alisema mgonjwa huyo aliugua kwa siku mbili ndipo madaktari wakalazimika kuchukua vipimo ili kujua kama ni ugonjwa huo.
“Baadaye wakati tukisubiri majibu ya vipimo kipindupindu, kikawa kimewagusa wengi na hadi kufikia Septemba 30, wagonjwa 16 wakaongezeka ambao wote ni waliopo wodini kwa ajili ya matibabu ya akili,” alisema Dk Charles.
Alisema hadi sasa hakuna mgonjwa aliyelazwa kwa ajili ya kuugua kipindupindu isipokuwa wapo wodini wanaendelea na matibabu ya ugonjwa wa akili.
Alibainisha hadi sasa chanzo cha ugonjwa huo hakijajulikana isipokuwa katika uchunguzi uliofanywa mgonjwa huyo aliyekuwa wa kwanza kuugua alitokea nje ya hospitali hiyo.
Kadhalika, alisema kumedhibitiwa muingiliano wa watu wanaotoka nje ya hospitali hiyo ikiwa ni pamoja na kusitisha huduma ya kupeleka chakula cha wagonjwa.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni