TIMU ya mpira wa kikapu ya wanawake ya JKT Star imefungwa vikapu 77-58 na KCCA ya Uganda kwenye michuano ya kanda ya tano ya mchezo huo inayofanyika kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa.
Kwa matokeo hayo, JKT Stars inashika nafasi ya tano kwenye msimamo kwa timu za wanawake, ikiwa na pointi tatu na KCCA ikiwa na pointi nne.
Kwenye mchezo mwingine, USIU ya Rwanda iliifunga Ubumbwe ya Rwanda pia vikapu 81-74, mchezo ambao ulikuwa na ushindani kwani hadi sasa timu hizo zina pointi sita zikitofautiana kwenye mabao ya kufunga na kufungwa.
Mchezo wa tatu, UCU ya Uganda iliifunga KPA ya Kenya vikapu 64 -60, kwa matokeo hayo UCU imefikisha pointi sita na KPA ina pointi tano.
Akizungumza na gazeti hili mmoja wa wasimamizi wa mashindano hayo, Haleluya Kalavambi alisema timu za Tanzania za wanawake na wanaume zinafanya vibaya na huenda zisifuzu kwenye robo fainali.
“Mashindano ni mazuri ila timu za Tanzania zinafanya vibaya kwenye hatua hii ya makundi na kuna dalili tusipate timu kwenye hatua ya robo fainali,” alisema Kalavambi.
Mashindano haya ya kanda ya tano kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati yalianza kutimua vumbi Oktoba mosi mwaka huu na yanatarajia kufikia tamati mwishoni mwa wiki hii.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni