TAARIFA HUKUJUZA MENGI YA ULIMWENGUNI

Jumatatu, 1 Agosti 2016

WAZIRI MKUU AMESEMA SERIKALI HAITASITA KUWAONDOA WAKURUGENZI WATAKAO TOA TAARIFA ZA UONGO

Hakuna maoni
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali haitasita kuwaondoa katika nyadhifa zao wakurugenzi wote watakaoshiriki katika kutoa taarifa za uongo kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.

Waziri Mkuu aliyasema hayo juzi jioni wakati akipokea taarifa ya Mkoa wa Morogoro mara baada ya kuwasili mkoani hapa kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.

“Serikali inatoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wakiandika taarifa za uongo kuwa mradi umekamilika wakati haujajengwa, hivyo wakurugenzi watakaoshiriki kutoa taarifa zisizokuwa sahihi wataondolewa,” alisema.

Alitumia fursa hiyo kutoa mwito kwa wakurugenzi katika halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatembelea miradi yote inayojengwa katika maeneo yao ili kufanya ukaguzi na kujiridhisha kama thamani yake inalingana na kiasi cha fedha kilichotolewa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliziagiza halmashauri zote nchini kufanya mapitio ya watumishi wa mikataba.

“Tumeruhusu kuajiri kwa mikataba walimu wa masomo ya sayansi kwa kipindi cha miaka miwili tena kwa waliostaafu. Kuna kada zilizoko katika muundo wa ajira hizo hatuhitaji watumishi wa mikataba wakiwemo madereva, msiwatumikishe kwa mikataba watakosa stahili zao,” alisema.

Akizungumzia suala la watumishi hewa mkoani Morogoro, alisema ni vema wakaendelea kufanya uchunguzi na ifikapo mwisho wa mwezi huu wawe wamekamilisha taarifa na kuanza kuchukua hatua kwa waliohusika

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni