TAARIFA HUKUJUZA MENGI YA ULIMWENGUNI

Jumatatu, 1 Agosti 2016

MAPYA YAIBUKA DODOMA , UGONJWA WAIBUKA HIVI KARIBUNI

Hakuna maoni


MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kituo cha Uchunguzi wa Magonjwa cha Marekani, katika utafiti wao, wamebaini ugonjwa uliobuka katika mikoa ya Dodoma na Manyara hivi karibuni na kuua watu, unasababishwa na sumu ya kuvu inayoshambulia ini.

Hadi kufikia Julai 31, mwaka huu, jumla ya wagonjwa 54 walisharipotiwa kuathiriwa na ugonjwa huo katika mikoa hiyo na kati yao 14 wameshapoteza maisha sawa na asilimia 20, hali ambayo Serikali imebainisha kuwa ni changamoto kubwa katika afya.

Hayo yalibainishwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu mwenendo wa hali ya ugonjwa huo katika maeneo yaliyoathirika.

Alisema tangu kuibuka kwa ugonjwa huo Serikali ilishirikiana na taasisi zake ikiwemo TFDA, Ofisi ya Mkemia Mkuu pamoja na wadau wa sekta ya kilimo na mifugo, mashirika ya kimataifa ikiwemo WHO na kuuchunguza kwa undani ugonjwa huo.

“Katika uchunguzi wetu tuliangalia nafaka hasa mahindi yaliyokuwa yanatumiwa na jamii iliyoathirika na tulibaini kuwa nafaka hizo zilikuwa zimeharibika kwa kubadilika rangi na kuoza, pia tumegundua jamii hizi, zimekuwa zikihifadhi vyakula kwa mtindo usioridhisha,” alisisitiza Ummy.

Alisema kati ya sampuli 115,52 sawa na asilimia 45 zilionesha kuwa na uchafu wa sumu ya kuvu kwa kiasi kisichokubalika kwa mujibu wa viwango vya kimataifa ambacho ni microgram isiyozidi tano kwa kilo moja ya nafaka.

Alieleza kuwa asilimia kubwa ya sampuli hizo zilipopimwa, zilionekana kuwa na uchafu wa sumu ya kuvu kwa kiwango cha microgram 5.7 hadi 204.5 kwa kilo moja ya nafaka.

“Hiki ni kiwango cha juu sana ikilinganishwa na kiwango kinachokubalika. Kiwango hiki kinafikia kinachoweza kusababisha ugonjwa sumu aflatoxicosis ambao hushambulia zaidi ini,” alisisitiza.

Alisema sampuli nyingine za binadamu, zilipelekwa kwenye maabara ya nje ya nchi jijini Antlanta nchini Marekani, ambapo kati ya sampuli 19 kati ya 24 zilizopelekwa nchini humo zilionyesha kuwa na viwango vya zaidi ya microgram 100 ya sumu ya kuvu.

Aidha Ummy alisema katika utafiti huo, wananchi wengine waliochukuliwa sampuli ingawa bado hawajaanza kuonyesha dalili za ugonjwa huo, nao walionekana kuanza kuathirika taratibu maini yao. Dalili za ugonjwa huo ni kuumwa tumbo, kuharisha, kutapika, tumbo kuvimba na mwili kuwa na rangi ya njano ishara ya ini kuathirika.

Akizungumzia hatua zilizochukuliwa hadi sasa na Serikali kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo, alisema wizara ya afya imeiagiza mamlaka ya TFDA kuendelea kuchunguza zaidi wilaya 10 za jirani na maeneo ili ugonjwa huo usienee.

Aidha alisema Serikali pamoja na kuendelea kutibia wagonjwa walioathirika, waliopo katika hospitali za mkoa wa Dodoma na wilaya ya Kondoa, pia inashirikiana na wadau wa kilimo na mifugo kutoa elimu kwa wananchi juu ya njia sahihi za kuhifadhi na kuandaa chakula.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo, alisema alitaja wilaya zilizoathiriwa zaidi na ugonjwa huo katika mikoa hiyo miwili kuwa ni Chemba yenye wagonjwa 38, Kondoa (9), Dodoma manispaa mmoja, Chamwino wawili na Kiteto watatu.

Akizungumzia ugonjwa wa kipindupindu, Ummy alibainisha kuwa bado ugonjwa huo haujadhibitiwa kikamilifu kwani na Dar es Salaam kutoripoti kuwa na mgonjwa wa ugonjwa huo tangu Mei 9, mwaka huu, manispaa ya Temeke jana iliripoti kupokea wagonjwa wapya wanne.

Alisema tangu ugonjwa huo uanze Agosti mwaka jana, jumla ya wagonjwa 22,375 waliripotiwa kuathirika kati yao watu wapatao 345 walipoteza maisha sawa na asilimia 1.5. Jumla ya wagonjwa waopya walioripotiwa wiki hii nchi nzima ni 44.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni