TAARIFA HUKUJUZA MENGI YA ULIMWENGUNI

Jumamosi, 30 Julai 2016

JESHI LA POLISI KANDA MAALUM YA DAR YAUA JAMBAZI HATARI

Hakuna maoni
Kamanda wa polisi kanda maalumuya Dar es salaaam Simon Sirro
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kikosi maalumu cha kupambana na majambazi, kimefanya msako na kufanikiwa kumuua jambazi hatari ambaye jina lake halikuweza kufahamika.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Simon Sirro alisema tukio hilo la kuuawa jambazi huyo lilitokea Julai 26 mwaka huu, maeneo ya Masaki Dar es Salaam.j
Alisema wakati askari wakiwa doria katika maeneo hayo, ghafla walisikia sauti ya mtu akiomba msaada huku akisema ‘Nakufa nakufa’ kutoka kwenye bajaji namba MC 754 AGV aina ya King ikiwa na watu wawili iliyokuwa katika mwendo kasi, ndipo askari walianza kuifukuza bajaji hiyo.
Mtu huyo alikuwa anataka kupora bajaji ya Ahmed Abdallah (38) mkazi wa Msasani Macho ambaye huwa anaegesha bajaji hiyo maeneo ya Oysterbay, Jackies Bar.

Alisema baada ya mtu huyo kuona wanafukuzwa na polisi alitoa bastola na kuwaelekezea askari, ndipo askari alimfyatulia risasi jambazi huyo iliyomjeruhi na kufanikiwa kumnyanga’nya bastola hiyo.

Majeruhi alikimbizwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo alithibitika kufa baada ya kufikishwa hospitali. Katika upekuzi, mtu huyo alikutwa na begi ambalo ndani kulikuwa na kisu kimoja, laini ya simu, simu ya mkononi aina ya Airtel, kadi ya chanjo yenye jina la S. Lipamba, risiti za benki ya DTB za kuweka pesa, tiketi ya basi ya Angel Liner ya kutoka Afrika Kusini kuja Dar es Salaam ya Mei 3, mwaka huu.

Katika tukio jingine, jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watu wawili wanaotuhumiwa kuwa ni vinara wa wizi wa magari na kukutwa na magari matatu ya wizi Jijini Dar es Salaam. 

alisema watu hao ambao ni Mulomba Kabamba ambaye ni dalali wa magari mkazi wa Mbezi alikamatwa na basi aina ya Tata lenye namba za usajili T 578 CGH na Toyota Carina lenye namba T 208 DCS.
Mtuhumiwa huyo akiwa na mwanamke walikodi teksi, Toyota Carina kutoka Feri kwenda Gongo la Mboto likiwa linaendeshwa na dereva Daud Daniel.

Aliongeza kuwa dereva huyo aliwaelezea tukio hilo ambapo alisema walipofika njiani walimtishia kisu na kumlazimisha kunywa dawa za kulevya na kupoteza fahamu, baadaye alijikuta ameokotwa huko Gongo la Mboto na kupelekwa Hospitali ya Amana akiwa amepoteza fahamu.

Alisema kikosi cha kupambana na wizi wa magari kilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo ambapo dereva teksi huyo alimtambua mtuhumiwa huyo ndiye aliyempora gari akiwa na mwanamke. Baada ya kutambuliwa mtuhumiwa alikiri kuhusika na tukio hilo na alimuuzia gari hilo, Alex Lyimo maarufu kwa jina la Papaa.

Kikosi hicho kilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo na katika mahojiano alikiri kupokea magari matatu kwa siku tofauti na mawili alikuwa tayari ameyauza mkoani Arusha na Kiteto mkoani Manyara.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni