TANZANIA imechaguliwa kuwa miongoni mwa nchi za Bara la Afrika
zitakazosaidiwa na China kuinua sekta zake za viwanda. Katibu Mkuu wa
Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk Adelhelm Meru, alisema hayo
jana wakati wa semina iliyoshirikisha wawakilishi wa taasisi mbalimbali
za serikali nchini, pamoja na wa China, ikihusu masuala ya ushirikiano
katika mageuzi ya viwanda.
Katika semina hiyo iliyofanyika Dar es Salaam juzi, Balozi wa China
nchini, Dk Lu Youqing alisema, nchi yake ina imani kubwa na Tanzania
katika suala zima la kukua kwa viwanda kutokana na rasilimali nzuri na
mazingira yake kuwezesha ustawi wa viwanda.
Alisema, katika nchi yoyote viwanda ndio vina nafasi ya pekee ya
kubadilisha uchumi na kuleta maendeleo kwa haraka. Alisema, kwa sasa
China ni miongoni mwa nchi zenye uchumi imara kutokana na kuwa na
viwanda vingi.
“Kupitia sekta ya viwanda, tunaweza kuboresha na kuimarisha kilimo
chetu, uchumi wetu na kujiletea maendeleo. China inazitia moyo nchi za
Afrika kupata maendeleo kupitia viwanda,” alisema.
Alisema, Tanzania inahitaji kuwa ya viwanda ingawa kuna changamoto
zinazoikabili, hivyo kuhitaji kutatuliwa. Aliongeza kuwa, asilimia 90 ya
nchi za Afrika zimeshajua umuhimu wa viwanda, lakini baadhi hazina
uwezo wala rasilimali za kuwezesha viwanda hivyo kufanya kazi.
Wakati huo huo, Dk Meru alisema, serikali itahakikisha sekta ya
viwanda inatoa asilimia 40 ya ajira nchini ifikapo mwaka 2020 na
kuchangia pato la taifa kwa asilimia 15, ifikapo mwaka huo.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni