MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imemnyima dhamana
aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry
Kitilya na wenzake wanaokabiliwa na mashitaka ya utakatishaji wa fedha.
Hakimu Mkazi Mkuu, Emilius Mchauru aliwanyima dhamana washitakiwa hao kwa kuwa mashitaka yanayowakabili hayana dhamana kisheria.
Akisoma uamuzi wa ombi la dhamana lililokuwa limewasilishwa na
washitakiwa hao kupitia kwa mawakili wao, Hakimu Mchauru alisema
mashitaka hayo hayana dhamana kisheria, pia kwa mujibu wa uamuzi
uliotolewa katika Mahakama Kuu, makosa ya utakatishaji wa fedha
yanaathiri uchumi, hivyo hayapaswi kutolewa dhamana.
Awali kabla ya kutolewa kwa uamuzi huo, mawakili wa washitakiwa hao
wakiongozwa na Wakili Alex Mgongolwa, waliiomba Mahakama waondoe ombi
hilo la dhamana walilokuwa wamewasilisha, lakini mahakama ilikataa na
kutoa uamuzi huo kwa sababu kwa kufanya hivyo wangezuia mahakama
isifanye kazi yake.
Baada ya kutolewa kwa uamuzi, Wakili Mgongolwa aliiomba mahakama
iwafutie washitakiwa shitaka la utakatishaji wa fedha kwa kuwa hati ya
mashitaka haina maelezo yanayokidhi vigezo vya kisheria vya shitaka
hilo, jambo ambalo lilizua mabishano ya kisheria.
Mgongolwa alidai ili shitaka liweze kuwa la utakatishaji wa fedha ni
lazima kuwe na hatua nne; kwanza kuwe na kuwekwa kwa fedha, kuhamishwa
kwa fedha na fedha kuwekwa kwenye shughuli za kiuchumi kwa lengo la
kuficha, pia kuwe na chanzo kichafu cha fedha.
Alidai katika maelezo ya mashitaka, upande wa Jamuhuri haujaeleza
hatua zote bali wametumia kifungu cha 12 (a) cha Sheria ya Kuzuia
Utakatishaji wa Fedha, ambacho kinagusia kuhamisha fedha tu badala ya
kutumia kifungu cha 12 a, b,c na d.
Hata hivyo, upande wa Jamuhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu,
Osward Tibabyekoma, ulipinga na kuomba mahakama itupilie mbali ombi
hilo kwa kuwa halina msingi kisheria na pia hati hiyo imekidhi maelezo
yote ya kosa la utakatishaji wa fedha.
Alifanunua kuwa, kosa hilo lina hatua tatu ambazo ni kuweka fedha,
kuhamisha na kuziweka kwenye shughuli za uchumi. Wakili Mgongolwa
alipinga na kudai, Wakili Tibabyekoma anapotosha na kuiomba mahakama
ikubali ombi lao na kufuta shitaka hilo.
Baada ya mabishano ya muda mrefu Hakimu Mchauru aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 22, mwaka huu atakapotoa uamuzi.
Washitakiwa walirudishwa rumande. Mbali na Kitilya washitakiwa
wengine katika kesi hiyo ni mrembo wa zamani wa Tanzania ambaye pia
alikuwa Mkuu wa Uwekezaji wa Benki ya Stanbic, Shose Sinare na aliyekuwa
Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa benki hiyo, Sioi Graham Solomon.
Mashitaka mengine yanayowakabili katika kesi hiyo mbali na
kutakatisha fedha, ni pamoja kutumia nyaraka za kughushi na za uongo
kujipatia isivyo halali Dola za Marekani milioni sita, sawa na Sh
bilioni 12 za Tanzania.
Wanadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Agosti 2012 na Machi 2013,
jijini Dar es Salaam, washitakiwa hao watatu walipanga pamoja kwa
kushirikiana na watu wengine ambao hawakufikishwa mahakamani hapo,
kutenda kosa la kujipatia fedha kwa udanganyifu kutoka serikalini.
Ilidaiwa kuwa kati ya Agosti 2, 2012 katika Makao Makuu ya Benki ya
Stanbic Tanzania Limited yaliyopo wilayani Kinondoni, Sinare akiwa na
nia ovu, alighushi taarifa ya maombi ya fedha ya Benki ya Standard ikiwa
na tarehe ya Agosti 2, 2012.
Kwa mujibu wa madai hayo, Sinare alieleza katika maombi hayo kuwa
Benki ya Standard ya London kwa kushirikiana na Benki ya Stanbic ya
Tanzania, watatoa mkopo unaofikia Dola za Marekani milioni 550 kwa
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa gharama ya asilimia
2.4 ya mkopo huo, wakati akijua kuwa gharama hiyo si kweli.
Inadaiwa kuwa, Agosti 13, 2012, mrembo huyo wa zamani wa Tanzania,
aliwasilisha taarifa hiyo ya kughushi katika Wizara ya Fedha iliyopo
Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam. Kwa mujibu wa madai hayo, Septemba 20,
2012 katika Benki ya Stanbic, Sinare alitengeneza na kuwasilisha barua
ya uongo ya kuelezea mkopo huo wa Dola za Marekani milioni 550, ikieleza
kuwa Benki ya Standard PLC kwa kushirikiana na Benki ya Stanbic,
zitatoa mkopo huo kwa Serikali kama wakikubaliwa.
Katika mashitaka mengine inadaiwa, Novemba 5, 2012 katika Benki ya
Stanbic jijini Dar es Salaam, washitakiwa wote watatu, wakiwa na nia
ovu, walitengeneza makubaliano ya uongo kwa lengo la kuonesha kuwa benki
imeipa kampuni ya Enterprise Growth Market Advisors (EGMA) Limited,
kazi ya kushughulikia mkopo huo.
Lengo la washitakiwa hao kwa mujibu wa madai hayo, lilikuwa
kufanikisha mkopo huo wa Dola za Marekani milioni 550 kwa Serikali ya
Tanzania, ambapo EGMA alitarajiwa kuonekana kuwa muongozaji wa
mazungumzo ya kupata mkopo huo.
Ilidaiwa kuwa Machi 2013 jijini Dar es Salaam, Kitilya, Sinare na
Sioi, wakiwa na lengo ovu walifanikiwa kupata Dola za Marekani milioni
sita, sawa na Sh bilioni 12, wakidai kuwa fedha hizo ni malipo ya kazi
iliyofanywa na EGMA Limited.
Katika shitaka la utakatishaji fedha wanadaiwa kati ya Machi 13 na
Septemba mwaka jana, kwa pamoja walitakatisha Dola za Marekani milioni
sita kwa kuzihamisha kwenda katika akaunti tofauti, kuzitoa katika
akauti hizo na kuziweka katika akauti nyingine tofauti zinazomilikiwa na
EGMA Limited katika Benki ya Stanbic Tanzania Limited na Benki ya KCB
Limited.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni