SERIKALI imesema inafanya juhudi za makusudi kuhakikisha kuwa watoto
wenye mahitaji
maalumu wanapata elimu sawa na wengine, ambapo mkazo wa
sasa ni kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.
Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Stella Manyanya, wakati
wa kuadhimisha Siku ya watu wenye usonji duniani, kwa niaba ya Makamu wa
Rais, Samia Suluhu Hassan, yalíyofanyika katika Shule ya Msingi ya
Al-Muntazir Upanga.
“Kwa sasa tunaendelea kuandaa walimu wenye ujuzi na maarifa ya elimu
maalumu, kuboresha miundombinu na huduma za kitabibu kwa ajili ya
kuwahudumia watoto wenye usonji na mahitaji maalumu kwa ujumla,”
alisema.
Aliitaka jamii kuwachukulia watoto wenye mahitaji maalumu kama sehemu
ya jamii na kuwashirikisha katika nyanja zote za maendeleo. Pia
aliwataka wazazi, walezi na jamii kuwapa kipaumbele bila kujali tofauti
za kimaumbile na kuhakikisha wanapata fursa ya elimu.
Alisema usonji ni upungufu wa kibayolojia anaompata mtoto anapokuwa
tumboni mwa mama yake na dalili zake huonekana kuanzia umri wa miaka
mitatu na kuendelea. Alisema kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani
(WHO), wamepima kila watoto 160, wanaozaliwa duniani mmoja anakuwa na
usonji.
“Watoto hawa wakipata maarifa na stadi za kuwawezesha kujumuika na
kujitegemea watapunguza hali ya utegemezi na kutoa fursa kwa wazazi na
wao wenyewe katika kujitafutia maendeleo,” alisema.
Alisema katika jamii ya kitanzania uelewa wa jamii bado ni mdogo na
huduma inayotolewa kwa watu wenye usonji si ya kuridhisha ambapo
wanakuwa na fikra potofu na imani za kishirikina na kwamba ni miongoni
yanayotajwa kukwamisha juhudi za kitabibu kwa watoto hao.
Aidha, alisema vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika
kuelimisha na kuhamasisha wazazi, walezi na jamii kwa ujumla ili
isiwafiche au kuwanyanyapaa watoto wenye ulemavu, badala yake watumie
fursa zilizopo ili kuhakikisha kuwa watoto wanapata haki za msingi
ikiwemo elimu.
Alisema serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi na wadau wa elimu
imekuwa ikipanua fursa za upatikanaji wa elimu kwa watoto wenye mahitaji
maalum kwa kuandaa walimu, kuboresha miundombinu kwa wanafunzi wenye
mahitaji maalumu katika elimu.
Alishukuru uongozi wa Taasisi ya Khoja Shia Itha Asheri Jamaat (KISJ)
kwani imekuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia watoto wenye usonji na
mahitaji mengine maalumu kwa kuwapa elimu na huduma nyingine za jamii.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni