TAARIFA HUKUJUZA MENGI YA ULIMWENGUNI

Alhamisi, 27 Oktoba 2016

TSN WADHAMINI TAMASHA LA MAGARI

Hakuna maoni

KAMPUNI ya Magazeti ya Serikali (TSN) inayochapisha magazeti ya Daily News, Sunday News, HabariLeo, HabariLeo Jumapili na SpotiLeo, itakuwa miongoni mwa wadhamini wa Tamasha la Magari Tanzania (Autofest) mwaka huu, ukiwa ni msimu wa tisa wa tamasha hilo.
Akizungumzia udhamini huo jana jijini Dar es Salaam, Meneja Mauzo na Masoko wa TSN, Januarius Maganga alisema wamedhamini upande wa habari na wametoa matangazo ya kutosha kuhusu tamasha hilo litakalofanyika viwanja vya Biafra, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Alisema katika tamasha hilo linalotarajiwa kufanyika kwa siku tatu kuanzia kesho, TSN itakuwa ikionesha bidhaa zake yakiwemo magazeti ya miaka ya nyuma yaliyosheheni habari zenye historia mbalimbali.
“Sisi kama Kampuni ya Magazeti ya Serikali tutakuwa pale na tutaonesha habari zetu, tutaonesha magazeti yetu na watu watajifunza mengi kuanzia miaka ya nyuma ikiwemo vita ya Kagera na Kesi ya Uhaini wanaweza kupata habari hizo na kujifunza mengi… Tuna hakika maktaba yetu inakidhi mahitaji ya wateja wetu,” alisema.
Mapema, Mratibu wa Autofest, Ally Nchahaga alisema mgeni rasmi katika ufunguzi wa tamasha hilo anatarajiwa kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage.
Alisema tamasha hilo litakuwa likionesha magari mapya, matoleo mapya ya pikipiki, burudani za kusisimua kwa ajili ya familia.
Alisema kwa sasa watu wengi wanashindwa kutunza vizuri magari yao kutokana na kukosa elimu, hivyo tamasha hilo limelenga kuendelea kuleta aina mbalimbali ya bidhaa ya vyombo vya moto na huduma ili wadau wajifunze, wafurahie na waridhishwe navyo.
Aliongeza kuwa, mbali na maonesho hayo, pia mwaka huu kutakuwa na uchangiaji wa damu.
Alisema pia kutakuwa na burudani mbalimbali na ujuzi wa kucheza na vyombo vya moto, na pia kutakuwa na eneo maalumu kwa ajili ya michezo ya watoto. Kiingilio katika tamasha hilo kitakuwa ni Sh 10,000 na kwa V. I. P Sh 40,000 kwa siku na tiketi za msimu itakuwa ni Sh 100,000.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni