KAMATI ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imekifungia kwa miezi mitatu kipindi cha Take One cha kituo cha televisheni cha Clouds, huku ikikionya kituo hicho kwa kukiuka kanuni za huduma za utangazaji.
Pamoja na adhabu na onyo, kituo hicho pia kimetakiwa kukitathmini kipindi cha Take One kwa lengo la kupata njia bora ya kukiendesha na kupeleka mapendekezo TCRA, kwa ajili ya kuridhia kabla ya kipindi hicho kufunguliwa.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Joseph Mapunda alisema jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa uamuzi wa kamati hiyo kuhusu lalamiko la ukiukaji wa kanuni za huduma za utangazaji kwa kituo hicho cha televisheni.
Agosti 9, mwaka huu kituo hicho kupitia kipindi chake cha Take One kilichorushwa hewani kati ya saa tatu na saa nne usiku na kurudiwa tena Agosti 10 kati ya saa saba na saa nane mchana, kilituhumiwa kutangaza maudhui yanayokiuka sheria na kanuni za utangazaji.
Alisema mtangazaji wa kipindi hicho, Zamaradi Mketema alifanya mahojiano na Gift Stanford `Gigy Money’ kwa kumuuliza maswali yaliyolenga masuala ya ngono na kumuongoza ataje majina ya wanaume aliofanya nao ngono, jambo ambalo linaingilia uhuru wa masuala binafsi ya watu kinyume na kanuni za huduma za utangazaji za mwaka 2005.
Mapunda alisisitiza kanuni za huduma za utangazaji zilizokiukwa kuwa ni ubora pamoja na staha, maadili ya jamii, kuepuka kuingilia faragha au maisha binafsi, kutoharibu ama kuchafua sifa za watu.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni