TAARIFA HUKUJUZA MENGI YA ULIMWENGUNI

Jumanne, 20 Septemba 2016

MBWA MWITU 22 WAUAWA KWA SUMU

Hakuna maoni

MBWA mwitu wapatao 22 wameripotiwa kufa kwa kile kinachodaiwa kulishwa sumu katika eneo la Kakesio linalotenganisha Hifadhi ya Ngorongoro na Pori la Akiba la Maswa.

Tukio hilo la kushtua limekuja wakati serikali, wataalamu wa uhifadhi pamoja na mashirika ya hisani wakiwa kwenye jitihada za kuwarejesha tena wanyama hao adimu ambao wanadaiwa kukaribia toweka duniani.

Kati ya mbwa mwitu hao, 11 waliuawa wiki iliyopita, wakijumlishwa na saba waliopewa sumu Mei mwaka huu pamoja na wale wengine 11 waliokufa Desemba mwaka jana, wanafanya idadi ya wanyama hawa adimu waliokufa hadi sasa kufikia 22.

Tayari kuna wageni kutoka nje wanaokuja nchini maalumu kuwaona mbwa mwitu tu, na mauaji ya wanyama hao yanahofiwa kuwa yataathiri sekta ya utalii. Na wakati mbwa mwitu 22 wakiripotiwa kufa huko Kakesio, wanyama wengine kama hao 11 waliokuwa kwenye kundi maalumu lililopewa jina la Osinoni wakipotea katika mazingira ya kutatanisha.

“Hawa wanyama walifungiwa vifaa maalumu vinatuvyowezesha sisi kuwafuatilia kwa satelaiti kokote wanakokwenda, lakini siku mbili zilizopita tumeviokota vifaa hivi katika bonde la Ubuntu,” alisema Martin Lomaiyani ole Pose ambaye ni Kiongozi wa askari wa wanyamapori kwenye Ukanda wa Kakesio.

Mtaalamu kutoka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI), Dk Ernest Mjingo alifafanua kuwa kundi la mbwa mwitu la Osinoni lilikuwa na wanyama 15, kati yao watoto saba na wakubwa wanane.

“Tumeokota mizoga minne ya wanyama wakubwa ila watoto saba hawajulikani walipo, lakini wakubwa wengine wanne tumewaona jana wakikimbia,” alisema Dk Mjingo na kuongeza kuwa wanyama waliofungiwa ‘Kola’ maalumu zenye vifaa vya satelaiti ni miongoni mwa waliokufa. “Hivyo ni vigumu sasa kuwafuatilia waliosalia kama wapo, maana katika kila kundi huwa tunawafungia ‘Kola,’ mbwa mwitu wawili tu ili kufuatilia kundi zima,” alisema mtafiti huyo na kufafanua kuwa kifaa kimoja huuzwa dola za Marekani 3,000 sawa na Sh milioni sita.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni