MAMLAKA
ya Mapato Tanzania (TRA) imetangaza kuanza kutembelea nyumba hadi
nyumba kuhakiki gharama za upangishaji ili kukokotoa na kukusanya kodi
sahihi ambayo ilikuwa haifiki serikalini.
Hivyo, wamewataka wananchi kutunza kumbukumbu za mikataba ya pango ili itakapohitajika na maofisa wa mamlaka hiyo wawapatie.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam jana wakati akielezea kuhusu makusanyo ya kodi kwa
mwezi Julai, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA,
Richard Kayombo alisema hatua hiyo ni moja ya mikakati ya kuongeza
ukusanyaji wa mapato.
Alisema
kwa Julai, TRA imekusanya Sh trilioni 1.055 sawa na asilimia 95.6 ya
lengo la kukusanya Sh trilioni 1.103 iliyopangiwa na serikali kwa mwezi
huo.
Alisema
ikilinganishwa na kipindi kama hiki kwa mwaka jana, TRA ilikusanya Sh
bilioni 914 ikiwa ni ongezeko la asilimia 15.43 ya makusanyo ya mwezi
huu huku kwa mwaka wa fedha 2016/2017, TRA imepewa lengo la kukusanya Sh
trilioni 15.1 ikilinganishwa na lengo la mwaka jana la Sh trilioni
13.32.
“Natoa
wito kwa wapangaji na wapangishaji kujiepusha na aina yoyote ya
udanganyifu katika suala zima la kodi halisi ya pango kwa kuwa inaweza
kuwasababishia kushtakiwa endapo udanganyifu huo utabainika,” alieleza Kayombo.
Kwa
sasa, wapangaji wengi hawalipi kodi serikalini baada ya kupanga nyumba,
na badala yake wamekuwa wakilipa fedha za pango kwa wamiliki wa nyumba
ambao wengi wao pia hawalipi kodi serikalini zaidi ya kulipia kodi za
majengo.
Wapangaji
wamekuwa wakilipishwa kodi ya pango kuanzia ya miezi sita hadi mwaka
moja na kodi hizo zimekuwa zikitofautiana kutokana na hadhi ya nyumba,
eneo ilipo, ukubwa wake na huduma ilizonazo kama maji na umeme.
Aidha,
Kayombo alisema pia mamlaka hiyo itatembelea waajiri katika maeneo
mbalimbali kuhakiki na kukagua usahihi wa orodha na malipo ya ajira ili
kujiridhisha kama kodi za ajira zinakokotolewa na kulipwa serikalini
inavyostahili.
Alisema
mbali na mkakati huo, TRA imeweka mikakati ya kuhakikisha walipakodi
wapya wanasajiliwa zaidi pamoja na kuhuisha taarifa za walipakodi kwa
kuhakikisha Namba za Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) zisizotumika
zinafutwa katika mfumo wa mamlaka.
“Maandalizi
ya kuhuisha taarifa za walipakodi yako katika hatua za mwisho
yakihusisha upigaji picha, kuchukua alama za vidole pamoja na vielelezo
muhimu vya mlipakodi ili kuhakikisha kila biashara inakuwa na TIN moja
tu yenye taarifa sahihi na za uhakika,” alifafanua.
Alisema
TRA imeboresha mifumo yake ili kupunguza au kuondoa changamoto za
kutopatikana kwa mtandao ambayo mara nyingi huathiri makusanyo ikiwa ni
pamoja na kuunganisha mifumo ya TRA na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari
Tanzania (TPA) ili kuhakikisha mapato ya serikali yanakusanywa kwa
usahihi na wakati.
Pia
wanaendelea kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato kwa kuhakikisha
wafanyabiashara wote wanaostahili kutumia mashine za kielektroniki za
kodi (EFDs) wanazitumia ipasavyo pamoja na kuwakagua wanunuzi wanapotoka
madukani kwa lengo la kuhakikisha wana risiti halali na sahihi kwa
manunuzi yao.
Kayombo
alisema TRA inawaasa wananchi kuhakikisha wanakagua risiti zao za
manunuzi na kuangalia usahihi wa fedha walizolipa na uhalali wa risiti
yenyewe.
“Tunatoa
wito kwa umma kutoa risiti wakati wa kuuza na kudai risiti wakati wa
manunuzi ya bidhaa au huduma kwani sheria ya fedha ya mwaka huu
imerekebisha sheria ya usimamizi wa kodi na wasiodai risiti kwa manunuzi
yoyote watapata adhabu ya Sh elfu thelathini hadi Sh milioni moja na
nusu,” alisema.
Alisema
kwa sheria hiyo kutotoa risiti na kutodai ni makosa kwa mujibu wa
sheria na hatua zitachukuliwa kwa wale watakaobainika kutotoa risiti au
kutodai risiti wakati wa mauzo na manunuzi.
Alisema
wanaendelea kukusanya mapato na kutoa elimu kwa wananchi hasa
mabadiliko ya sheria mbalimbali za kodi kama Sheria ya Fedha ya mwaka
2016 iliyopitishwa hivi karibuni ili kujenga uelewa na kukuza ridhaa ya
kulipa kodi kwa hiari.
Tangu
kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano, Rais John Magufuli
amekuwa akisisitiza Watanzania kujenga tabia ya kutoa na kudai risiti
kwa kusisitiza ‘ukinunua dai risiti na ukiuza toa risiti.’
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni