Raisi John Pombe |
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza
viongozi wote wa kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Kitongoji hapa nchini
kufuatilia matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kutoa
elimu bila malipo kwa lengo la kudhibiti mianya ya matumizi mabaya ya
fedha hizo.
Rais
Magufuli ametoa maagizo hayo leo tarehe 01 Agosti, 2016 katika mkutano
wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mnadani na kuwajumuisha wananchi
wa Katoro na Buseresere Mkoani Geita.
Katika agizo hilo Dkt. Magufuli amewaonya walimu ambao wameanza kufanya udanganyifu kwa kuandikisha idadi kubwa ya wanafunzi kuliko idadi halisi kwa
lengo la kupata mgao mkubwa wa fedha za ruzuku na amesema Serikali
itachukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayebainika kufanya hivyo.
"Ninafahamu
mgao wa fedha hizo hutolewa kulingana na idadi ya wanafunzi waliopo,
wapo baadhi ya walimu ambao wameanza kuandika wanafunzi hewa katika
shule zao, ili kusudi aletewe hela nyingi kuliko idadi ya wanafunzi
waliopo, wanafunzi kama wapo laki nne yeye anasema shule yangu hii ina
wanafunzi laki tano, ili kusudi hela zikija za wanafunzi laki tano, za
wanafunzi laki moja wagawane.
"Napenda nitoe wito kwa walimu Tanzania nzima, mnatafuta matatizo, narudia mnatafuta matatizo, msijaribu kula hela ya Serikali" Amesema Rais Magufuli.
Pamoja
na agizo hilo, Rais Magufuli pia ametaka viongozi wa ngazi zote katika
Mikoa kuhakikisha wana takwimu za idadi ya wanafunzi katika shule zote
zilizopo katika maeneo yao ili kurahisisha ufuatiliaji wa fedha hizo na
amesema kuwa kuanzia sasa ataanza kutembelea shule kwa kushitukiza na
kwamba kiongozi atakayeonekana kutojua takwimu itakuwa ni uthibitisho
kuwa hatoshi kuendelea na wadhifa alionao.
"Na
nitoe wito kwa viongozi wa Mikoa, Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya,
Wakurugenzi, Makatibu Tarafa, Watendaji wa Kata, Wenyeviti wa Vijiji,
kila mmoja awe na idadi ya wanafunzi waliopo katika shule zao, hatutaki
kuwapunja wanafunzi hela ambayo wanatakiwa kupata, lakini pia hatutaki
kutoa hela ambayo haitakiwi" Amesisitiza Rais Magufuli.
Mhe.
Rais Magufuli ambaye ametumia mkutano huo kueleza juhudi mbalimbali
zilizofanywa na Serikali yake ya Awamu ya Tano, kutekeleza ahadi yake ya
kujenga Tanzania Mpya pia amewataka viongozi na watendaji wa Serikali
kutekeleza wajibu wao kwa kutembelea wananchi wanaowaongoza badala ya
kukaa muda mwingi ofisini huku akisisitiza ofisi hizo kuwepo katika
maeneo yenye shughuli husika.
Aidha,
Dkt. Magufuli amekosoa utaratibu unaotumiwa na Halmashauri nyingi za
Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya kutumia mawakala katika ukusanyaji wa
mapato ya Halmashauri akisema mawakala hao wamekuwa wakitumia utaratibu
huo kukusanya fedha nyingi na kisha kuwasilisha kiasi kidogo katika
Halmashauri husika.
"Hivi
kwa nini Halmashauri msingekuwa na maafisa wenu wazuri na mkawa na
mashine za kielektroni kwa ajili ya kukusanya fedha? Amehoji Dkt.
Magufuli na kuongeza kuwa;
"Tena
mawakala wengine ndio hao hao wamekuwa wakikusanya kodi hata kwa
wananchi wanyonge wenye vibiashara vidogo vya kuuza mchicha bila hata
kuwaonea huruma"
Rais
Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amemaliza
ziara yake ya siku nne katika Mikoa ya Singida, Tabora, Shinyanga na
Geita na yupo nyumbani kwake Chato Mkoani Geita kwa mapumziko mafupi.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni