Jumatano, 10 Agosti 2016
NAPE : ANDIKENI HABARI NJEMA KUHUSU AFRIKA
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amesema ipo haja kwa vyombo vya habari vya Afrika kuandika habari zilizo njema zinazohusu bara hilo na taarifa hizo zifikie nchi za magharibi ili nchi hizo ziwe na maono chanya juu ya Afrika.
Alisema hivyo jana Dar es Salaam wakati alipozungumza kwenye kongamano la kidiplomasia kati ya China na Afrika.
Alisema suala hilo ni changamoto kubwa kwa vyombo vya habari kwani mara nyingi vimekuwa vikiandika kama hakuna jambo jema katika bara la Afrika.
“Vyombo vya habari viandike yale yaliyo mema ya Afrika na kuhakikisha taarifa hizo zinazungumzwa duniani, wenzetu wamekuwa wakitumia vyombo vyao kuandika taarifa chanya za nchi zao,” alisema Nape.
Alisema haitoshi kwa vyombo hivyo kuandika kwa ajili ya wenyewe kwa wenyewe, bali wapenye kwa kuhakikisha habari hizo zinafika katika maeneo ya nchi nyingine ili nao wajue Afrika inafanya yaliyo mema na sio kubaki na mtizamo kuwa bara hilo halina lililo jema.
Kwa upande mwingine, alizungumzia kongamano hilo linaloonesha nia ya China kuwekeza katika Bara la Afrika katika nyanja ya mawasiliano na kusema kuwa ni moja ya jitihada za kuboresha sekta hiyo, kuongeza uzoefu walio nao na namna wanavyoshughulika na dunia kupitia mawasiliano.
Alisema kwa kupitia uwekezaji huo katika eneo la mawasiliano, vyombo vya habari vitaweza kuboreshwa katika nyanja mbalimbali na kuzitaka nchi za Afrika kuwa tayari kutumia fursa hiyo kwa ajili ya kukuza uchumi na kuleta maendeleo.
Kuhusu namna China ilivyoweza kuimarisha utamaduni wake kwa kukuza uchumi, alisema jambo la kujifunza ni mambo gani waliyoyatumia hasa kwa kujenga uchumi wao ili Bara la Afrika liyatumie na kupiga hatua kutoka walipo na kukuza uchumi zaidi
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni