KATIBU Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk Adelhem Meru, amewataka viongozi wa Serikali za Mitaa nchini kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vidogo.
Meru alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati wa hafla fupi ya kuorodhesha hati fungani za Benki ya NMB kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) zenye thamani ya Sh bilioni 41.4.
Dk Meru alisema tayari serikali imejipanga kujenga viwanda hivyo katika kila mtaa hivyo ni muhimu kwa viongozi hao kuhakikisha wanatenga maeneo katika mitaa yao ili ujenzi huo utakapoanza kuwepo tayari na maeneo.
Ameiomba benki hiyo kupunguza riba ya fedha hizo walizozipata ili kuwasaidia wafanyabiashara wengi hasa wafanyabiashara wadogo na wa kati kupata mikopo yenye gharama nafuu.
Aliongeza kuwa kupunguzwa kwa riba hizo kutasaidia pia wafanyabiashara kukopa fedha kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vidogo vidogo.
“Tunaamini benki yetu ya NMB itatufikiria katika suala hili, riba zinazotolewa kwa sasa ni kubwa na sio rafiki kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati. Pia tutajitahidi kuzungumza na benki nyingine ili nao watusaidie kupunguza riba hizo kwa wafanyabiashara wetu ili kuleta maendeleo na kuongeza pato la nchi,” alisema Dk Meru.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni