TAARIFA HUKUJUZA MENGI YA ULIMWENGUNI

Jumanne, 19 Julai 2016

MOTO WAUNGUZA KIWANDA CHA 21ST CENTURY TEXTILES LIMITED

Hakuna maoni
KIKOSI CHA ZIMAMOTO WAKIWA KATIKA HARAKATI ZA KUZIMA MOTO KATIKA KIWANDA MKOANI MOROGORO


 VIKOSI vya askari wa Jeshi la Uokoaji na Zimamoto, Polisi na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kambi ya Mzinga vimeunganisha nguvu kuzima moto mkubwa uliokuwa ukiteketeza jengo la Idara ya Uzalishaji katika kiwanda cha 21st Century Textiles ( 1998) Limited mkoani humo.

Moto huo katika kiwanda hicho kilichojulikana zamani kama ‘Polytex’, kilichopo kwenye eneo la viwanda vya Kihonda, ulianza kuwaka jana saa 12:45 asubuhi na haukuweza kuzimwa hadi saa 9:00 alasiri.

Kamanda wa Kikosi cha Uokoaji na Zimamoto mkoani humo, Ramadhan Pilipili, alisema licha ya kuwahi katika eneo la tukio, walishindwa kuingia kwa urahisi ndani ya kiwanda hicho, hivyo kulazimika kutoboa ukuta ili kurusha maji ndani kwa lengo la kuzima moto huo.

“Ndani ya jengo hilo kulikuwa na marobota ya pamba yaliyokuwa yakiwaka moto, haikuwa rahisi kuingia lakini tulilazimika kutoboa ukuta na kupenyeza maji ili kuuzima moto,” alisema Pilipili.

Alisema timu ya askari kutoka JWTZ, kambi ya Mzinga mkoani hapo iliungana nao kuzima moto huo. Katika tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Ulrich Matei alishiriki kuzima moto huo pia na kudhibiti usilete madhara makubwa zaidi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa huo, Dk Stephen Kebwe aliyefika kwenye tukio aliuagiza uongozi wa Kikosi cha Uokoaji cha Zimamoto mkoa kufanya ukaguzi mara kwa mara kiwandani hapo. Alisema lengo ni kujiridhisha kuwa viwandani kuna vifaa vya dharura vinavyofanya kazi ya kuzima moto pindi unapozuka.

“Maeneo kama haya ya viwanda ni lazima kuwepo na vitu vya tahadhari , kama sehemu za kuchota maji , vifaa vya kuzimia moto viwemo ndani ya viwanda na maeneo mengine ili moto unapozuka iwe ni rahisi kuwahi kuuzima,” alisema Dk Kebwe.

Mbali na hayo, Dk Kebwe alimwagiza Kamanda wa Polisi wa mkoa kuimarisha ulinzi kwenye eneo hilo, ili kuzuia vibaka na wezi wasiibe mali zilizopo.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni